Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa Jubilei Miaka 50 ya Daraja Takatifu ya Upadre
Askofu Tarcisius J.M. Ngalalekumtwa anawaalika Mapadre kumtazama na kumtafakari Kristo Yesu aliyejitoa kama: Mwalimu, Mchungaji na Kiongozi, akaonesha uaminifu, utii na upendo usiokuwa na mipaka kwa waja wake. Uaminifu wa Kristo uwe ni changamoto ya uaminifu wa Mapadre unaojionesha kwa namna ya pekee katika: upendo, unyofu, unyenyekevu, huruma na huduma makini kwa watu wa Mungu. Kanisa linawahitaji walezi makini katika majiundo ya kipadre.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Askofu Tarcisius J.M. Ngalalekumtwa Jumatatu tarehe 17 Aprili 2023 ameadhimisha Jubilei ya Miaka 50 tangu alipopewa Daraja Takatifu ya Upadre na Miaka 34 ya Uaskofu akiendelea kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Katika mahojiano maalum na Radio Vatican, anawaalika watu wa Mungu nchini Tanzania kusali na kuombea miito mitakatifu ndani ya Kanisa kwani kuna majimbo ambayo yamebahatika kuwa na waseminari wengi, lakini kuna majimbo mengine yana ukame wa kutisha wa waseminari. Jambo la msingi ni kuliombea Kanisa ili liweze kuwapata walezi bora, makini na wenye moyo wa kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya Kanisa la Tanzania na Ulimwengu katika ujumla wake. Mapadre walezi wawe ni mfano bora wa kuigwa kama alivyokuwa Kristo Yesu, Kuhani mkuu na wa milele. Lengo ni kuwaandaa Majandokasisi, watakaoweza kutenda kazi katika shamba la Bwana, ili Mwenyezi Mungu atukuzwe, mwanadamu atakatifuzwe na hatimaye, kupata wokovu kupitia mikononi mwa wachungaji wema na watakatifu. Ili kufikia azma hii, kuna haja ya kuwa na walezi bora pamoja na mahitaji msingi yatakayowezesha kufanikisha azma hii katika maisha na utume wa Kanisa.
Askofu Tarcisius J.M. Ngalalekumtwa anawaalika Mapadre kumtazama na kumtafakari Kristo Yesu aliyejitoa kama: Mwalimu, Mchungaji na Kiongozi, akaonesha uaminifu, utii na upendo usiokuwa na mipaka kwa waja wake. Uaminifu wa Kristo uwe ni changamoto ya uaminifu wa Mapadre unaojionesha kwa namna ya pekee katika: upendo, unyofu, unyenyekevu, huruma na huduma makini kwa watu wa Mungu. Mapadre wajitahidi kuwa ni watu wenye mvuto si kwa sababu ya kuwapendeza watu, bali kutokana na unyofu wa maisha yao, unaowafanya kuwa kweli ni vyombo kwa waamini kuweza kumkimbilia Mungu na Kristo wake. Mapadre wajitahidi kumtazama Kristo kama mfano na kielelezo cha kuigwa. Watambue kwamba, Yesu ndiye mwalimu na mlezi mkuu wa Mapadre wanaoendeleza huruma takatifu kati ya watu wake. Padre ni ufunguo wa malango ya huruma, msamaha na upendo wa Mungu kwa binadamu! Ikumbukwe kwamba, wito na maisha ya Upadre ni neema na zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu inayopaswa kumwilishwa katika fadhila ya huruma na mapendo kwa Mungu na jirani. Kristo Yesu katika maisha na utume wake alijisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kutangaza Habari Njema ya Wokovu na kusimika Ufalme wa Mungu unaofumbatwa katika misingi ya haki, amani, upendo na mshikamano. Akawachagua Mitume wake kumi na wawili ili kusaidia mchakato wa uinjilishaji, huku wakisaidiwa na wafuasi wengine 72 waliotumwa kwenda kumwandalia Kristo Yesu, mazingira ya uinjilishaji.
Alhamisi Kuu, siku ile iliyotangulia kuteswa kwake, Kristo Yesu aliweka Sakramenti ya Ekaristi Takatifu na Daraja Takatifu, kielelezo cha huduma makini inayomwilishwa katika Injili ya upendo na huduma. Yesu aliwapatia Mitume wake jukumu la kuwa ni: Manabii ili wahubiri Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa Mataifa; Makuhani ili waweze kuwatakatifuza Watu wa Mungu kwa sala, sadaka na ushuhuda wa maisha yao; na Wafalme kwa kuwaongoza watu wa Mungu. Askofu Tarcisius J.M. Ngalalekumtwa wa Jimbo Katoliki la Iringa, Tanzania alizaliwa tarehe 25 Oktoba 1948. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, tarehe 17 Aprili 1973 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre kwa ajili ya Jimbo Katoliki la Iringa. Tarehe 14 Novemba 1988 akateuliwa na Mtakatifu Yohane Paulo II kuwa Askofu mwandamizi mwenye haki ya kurithi Jimbo Katoliki la Sumbawanga. Tarehe 6 Januari 1989 wakati wa maadhimisho ya Sherehe ya Ufunuo wa Bwana, Epifania, akawekwa wakfu na Mtakatifu Yohane Paulo II, kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Tarehe 21 Novemba 1992 akateuliwa na Mtakatifu Yohane Paulo II kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Iringa. Jumatatu tarehe 17 Aprili 2023 anaadhimisha Jubilei ya Miaka 50 tangu alipopewa Daraja Takatifu ya Upadre na Miaka 34 ya Uaskofu akiendelea kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu.
Jubilei Iringa