Masista Wamisionari Waconsolata Kuadhimisha Jubilei Ya Miaka 100 Tanzania Januari 30,2023
Masista wa Shirika Kitawa Bikira Maria Consolata (M.C) ifikapo Januari 30,2023 wataadhimisha Jubilei ya miaka 100 ya Shirika lao tokea wafike nchi ya Tanzania.
Akiongea na Kiongozi hivi karibuni Mama Mkuu upande wa malezi kwa nchi ya Tanzania Sr. Hortensia Damian (M.C) amesema kuwa, shirika hilo lilianzishwa mwaka 1910 nchi ya Italia Torino na Mwenye Heri Yosefu Alamano.
“Shirika liliendelea kuku ana hadi kufika katika Nchi ya Tanzania mnamo mwaka 1923, na katika Jimbo la Iringa wamisionari wetu walifika katika Parokia ya Tosamaganga wakitembea kwa miguu kutoka Bihawana – Dodoma, walipofika wakikumbana na upinzani wa kutoka imani za kijadi mfano waganga wa kienyeji, uchawi, familia zenye mitara, kuozwa kwa mabinti wadogo, kutopelekwa shuleni watoto, na wengine wakiumwa walikuwa hawaendi hospitalini wanapoumwa na pia masista wetu waliugua magonjwa yaliyowapelekea kifo, hapa tunaona ni jinsi gani walivyokuwa na moyo wa kimisionari kwani hawakukata tamaa.” amesema Sr. Hontenisia.
Kwa mujibu wa Sr. Hortensia amesema kwamba, lengo la mwanzilishi wa Shirika hilo lilikuwa ni kuhibiri Injili kwa watu wote wasiomjua Yesu Kristo Faraja ya kweli akilenga hasa bara la Afrika.
Pamoja na kuadhimisha miaka 100 Sr. Hortensia anasema bado kuna changamoto mbalimbali kwa waamini kwa sababu bado baadhi ya waamini hawabaki katika Imani yao wanahama hama Kwenda madhehebu mengine.
Tunaadhimisha miaka 100 ya shirika letu la kitawa, lakini bado kuna changamoto mbalimbali Pamoja na kuhama kutoka kwenye Imani ya kanisa letu katoliki, bado kuna Imani za kishirikina, uchawi watu hawamwini Yesu tena, waamini hawaendi kanisani wanabakia majumbani mwao”amesema Sr. Hortensia na kuongeza kuwa “bado pia kuna changamaoto ya wakristo kujiingiza kwenye ‘ufreemason’ wakitafuta zaidi utajiri na kuacha kabisa kufanya kazi wakitegemea vitu kama hivyo”.
Pamoja na changamoto hizo lakini shirika hilo la kitawa limekuwa na mafanikio mbalimbali ikwepo kuenea kwa ukristo maeneo mengi ambako wanafanya utume, wamepatikana maaskofu wazalendo, watawa wakike na kiume.
Wamisionari hao pia Pamoja na kuleta injili kwa watu wote, masista hao pia wamefanikiwa kufungua vituo vya afya, shule za awali na sekondari.
Mama mkuu huyo amewataka watanzania kwa ujumla kutunza amani iliyopo isipotee washikamane kwa umoja ili waendelee kulijenga Taifa lao.
Nae Sr. Salesia Mgaya (M.C) ambaye anasimamia Jimbo Katoliki la Njombe upande wa shirika lao amesema kuwa katika utume wake amejifunza kuwa tayari kufanya utume katika mazingira yoyote
“Katika kipindi chote hiki tumeshuhudia ustawi wa makanisa yetu, Sinodi imeleta watu kujitegemea Zaidi kuliko kusubiri misaada kutoka nje ya nchi, lakini pia katika utume wangu nimejifunza kuwa tayari kufanya kazi mazingira yoyote yale” amesema Sr. Mgaya.
Akizungumiza suala la maadili kwa vijana, Sr Mgaya amesema kwamba, kuna mmomonyoko wa maadili kwa vijana lakini pia amesikitishwa na suala la wazazi kutoshiriki kikamilifu katika kuwalea watoto wao lakini ukikuta suala la ‘kujipamba’ huweza kufanya hivyo.
“Mmomonyoko wa maadili haukubaliki kamwe, na tutambue kwamba tulishasaidiwa sana katika kuimarisha Imani yetu, sasa ni zamu yetu kutoa na kutumika, kuwa waaminifu pia katika majukumu yetu, Imani tumeipokea bure tutoe bure” amesisitiza Sr. Mgaya na kuongeza kuwa “Waamini kwa umoja wetu tuchangie ghrama za malezi katika kulea miito mitakatifu, tusiseme hakuna miito, miito ipo tuilee kwa Pamoja na sio kuwaachia wanashirika peke yake”
Kwa upande wake Sr. Idelfonsia Kihaka ambaye anafanya utume wake katika Nchi ya Colombia amesema kwamba kuna ubaguzi wa rangi kati ya wahindi wekundu na wazawa wa nchi hiyo tofauti na nchi ya Tanzania.
“Utume wetu zaidi ni porini na sio mijini, tumebarikiwa sana katika nchi yetu hakuna matabaka yoyote ila katika nchi ya Columbia matabaka yapo kabisa wanabaguana kulingana na rangi zao”amesema Sr. Kihaka.
Sr. Luisella Bensone yeye ni mzaliwa wa Italia na utume wake ameanza nchi ya Tanzania kuanzia mwaka 1978 amesema kuna utofauti mkubwa wa kiimani na maendeleo yanaonekana watu wameelimika na pia nchi imesonga mbele.
“Nilifika mwaka 1978, maendeleo sasa ni makubwa, watu wameelika nchi inasonga mbele sio upande wa shule tu hata maeneo mengine pia yamekuwa vizuri, wito wangu tuendelee kujivunia amani tuliyonayo toka akiwepo Mwalimu Nyerere hadi waliopo, hatuna vita, tuendelee kuitunza amani yetu” amesema St. Luisella.
Shirika hilo linapoadhimisha miaka hiyo 100 nchini Tanzania, linajivunia kupata wazao wamisionari wa Consolata ambao walio wengi wanafanya utume wao nchi za nje wakiinjilisha katika mabara ya Ulaya, Afrika, Amerika na Asia.
Pia wanafanya utume wao katika majimbo Katoliki matano ambayo ni Iringa, Morogoro, Lindi, Jimbo Kuu Katoliki Dar es Salaam na Dodoma.
Anayehitaji kujiunga na shirika lao anatakiwa awe na Imani ya Kikatoliki mwenye wito wa kimisionari, aliyehitimu kidoto cha nne Pamoja na kozi isiyopungua miaka miwili, kidato cja sita au chuo.
Kilele cha maadhimisho ya Jubilei hiyo itaadhimishwa kwenye Kanisa la Bikira Maria Consolata Parokia ya Mshindo Januari 30 mwaka huu 2023 ambako itahudhuriwa pia na maaskofu, mapadre, watawa wa mashirika mbalimbali yaliyopo jimboni Iringa na nje ya Jimbo Pamoja na waamini walei wenye mapenzi mema.