Jimbo Katoliki Iringa lapata Mashemasi watatu (3)

ASKOFU Tarcisius Ngalalekumtwa wa Jimbo Katoliki la Iringa ametoa daraja Takatifu la ushemasi kwa mafrateli 3 wa jimbo hilo na kuwataka kuwa wacha Mungu, wanyenyekevu, wasafi na wenye roho ya huruma.

Misa ya kutoa daraja hilo imefanyika katika Kanisa la Kiaskofu la Moyo Mt. wa Yesu  Parokia ya Kihesa na kuhudhuriwa na mapadre, watawa kike na kiume pamoja na waamini wenye mapenzi mema.

Waliopata daraja hilo ni Pamoja na Frateli Benobili Kisaka wa Parokia ya Mbarali, Emanuel Liwehuli (Kitanewa) na Frateli Emanuel Myovela wa Parokia ya Kihesa.

Akitoa homilia yake askofu Ngalalekumtwa amesema kwamba mashemasi hao wanatakiwa kuwa chombo safi mikononi mwa Kristo kwa utakaso wao, watunze useja wao ili wapate kutumika kwa Mungu na watu kwa moyo usiogawanyika wakisali katika sala.

“Watu wawakute wapo mbele ya Ekaristi wakisali na kukesha, mjuwe na bidii kujali muda wenu katika matedo ya huruma” amesema askofu Ngalalekumtwa.

Aidha amesema kuwa mashemasi pia ni watu wa huduma ya Mungu, wanapewa jukumu la Imani na kuongoza sala “Mnatunukiwa daraja hilo kama zawadi bora,skaramenti ya huduma takatifu katika ngazi ya ushemasi ni hatua ya kuelekea kwenye upadre”

Askofu Ngalalekumtwa amesema, Kanisa limeendeleza karama hiyo kusudi wawepo wawe msaada kwa askofu na mapadre katika huduma ya Neno na kuwagawia watu mwili wa Bwana katika Kanisa.

Amesema mashemasi hao wanapewa jukumu kuu hilo, walimu wa Imani, wajumbe wa Yesu Kristo na katika daraja hilo pia wataongoza ala, watabatiza, kusimamia na kubariki ndoa, kupeleka komunyo kwa wagonjwa na wataongoza ibada ya mazishi.

Misa hiyo ya daraja la ushemasi imeongozwa na askofu Tarcisius Ngalalekumtwa mwanzoni mwa juma wakiwepo pia na mapadre wa Jimbo na mapadre kutoka mashirika mbambali ya kitawa yaliyopo jimboni hapa.

Similar Posts