Maadhimisho ya Misa ya Kuwaombea Marehemu

 

Mhashamu Baba Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa wa Jimbo Katoliki Iringa akisimika msalaba kwenye kaburi la Padre Camillo (IMC) kwenye shamba la Mungu lililopo Parokia ya Tosamaganga.

Askofu Tarcicius Ngalalekumtwa, amewaongoza waamini wa jimbo la Iringa katika Misa Takatifu ya kuwaombea marehemu maaskofu, mapadre watawa wa kike na kiume pamaja na waamini walei wa Jimbo. Misa hiyo imefanyika kwenye kanisa la Moyo Mtakatifu wa Yesu Parokia ya Tosamaganga, na mara baada ya Misa hiyo askofu Ngalalekumtwa pamoja na baadhi ya mapadre wameyabariki makaburi yaliyopo kwenye shamba Mungu Tosamaganga.

Akitoa homilia yake askofu Ngalalekumtwa amesema kwamba waamini watambue kwamba hekima ya Mungu inawafundisha kuwa hapa duniani ni mapito, mahali pa kukesha na hawapaswi kujisahau na kubweteka na mambo ya dunia.

 

Sehemu ya eneo la shamba la Mungu, Tosamaganga.

“Dunia hii ni batili, tambala bovu, tudumu katika Imani yetu, tusiende kufukua makaburi ya baba zetu ni kufuru tuache hiyo tabia, haipendezi tunaposikia kwamba waamini wanaenda usiku kufukua makaburi!” amesema askofu Ngalalekumtwa  na kuongeza kuwa

“ Twende tukawatembelee wapendwa wetu sio kwa ajili ya kukata mafundo hapana, bali kuwaombea, tuwaache walale kwa amani, tunahimizwa kufanya hija kutembelea kule wenzetu walipolala kuwahakikishia kwamba tunawaombea”.

Askofu Ngalalekumtwa amesema kwamba, wanadamu wameumbwa kwa ajili ya Mungu na wapo safarini kama mahujaji, wapita njia wanakesha wakitanzamia ujio wa pili wa Bwana Yesu atakaporudi katika ukuu na kuufanya upya.

“Hapa leo tumekusanyika kusudi kuwakumbuka wapendwa wetu na wote duniani waliolala katika usingizi, tunawaombea katika upendo mkubwa ili Mungu awatakase na tunamuomba kusudi baada ya utakaso wao, huruma na upole wa Mungu udhihirike kwao, waweze kupokea heri ambayo waliitamani walipokuwa hapa duniani” waweze kujipatia Faraja waliokuwa wakiitafuta hapa duniani”.

Askofu Ngalalekumtwa amesema kwamba mwezi Novemba ni mwezi wa kipekee waamini wanaalikwa kutoa sadaka, maombi na maombolezo na kuwakumbuka waliokwisha aga dunia lakini bado hawajaingia Mbinguni, wanahitaji utakaso, Mungu wa Mbinguni afupishe safari yao ili waingie katika bwalo la Bwana pale ambapo Faraja hiyo wataipokea wakiwa kifuani mwa Baba yao Ibrahimu.

Zaidi ya mapadre 50, watawa wa kike na kiume Pamoja na walei wenye mapenzi mema wamehudhuria Misa hiyo.

Pia unaweza kufuatilia mahubiri ya Ask. Tarcisius Ngalalekumtwa katika channel ya Jimbo Katoliki Iringa Online TV.

https://youtu.be/0iZFjWEGzOQ
Mhashamu Baba Askofu Tarcicius Ngalalekumtwa wa Jimbo Katoliki Iringa akitoa homilia kwenye Misa Takatifu ya kuwaombea marehemu Maaskofu, mapadre, watawa na waamini walei wa Jimbo hilo.

Kumbuka Kushirikisha wengine, ku Like, Comments na Ku subscribe channel yetu ya Jimbo Katoliki Iringa.

Mwisho.

Similar Posts