|

Jimbo Katoliki la Iringa lapata mapadre wapya wanne (4) .

Daraja Takatifu la Upadrisho limetolewa na Mhashamu Baba Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa wa Jimbo  Katoliki la Iringa ambako ibada  imefanyika kwenye viwanja vya Kanisa Kuu la Kiaskofu la Moyo Mt. Wa Yesu Parokia ya Kihesa, siku ya Alhamisi tarehe 26, Agosti 2021.

Adimisho hilo lilitanguliwa na ibada ya masifu jioni ambapo mashemasi hao waliweka viapo siku ya Jumatano jioni.

Waliopata daraja hilo ni Shemasi Florence Ngerangera wa Parokia ya Usokami, Shemasi Gelasius Mwalongo- kutoka Parokia ya Ujewa, Shemasi Mathew Kilamlya wa Shirika la Bikira Maria Consolata kutoka Parokia ya Ilole na Shemasi Nelson Fungo kutoka Parokia ya Kaning’ombe. Katika homilia yake Mhashamu Baba Askofu Ngalalekumtwa amewataka mapadre hao wapya kuihubiri Injili kwa uaminifu, kulichunga Taifa la Mungu, kuongoza sio kwa kuonyesha mkono bali kwa mwenendo wao na kuziadhimisha Ibada Takatifu.

Pichani kutoka Kulia: Pd. Nelson Fungo , Pd. Mathew Kilamlya IMC, Pd. Florence Ngerangera, na Pd. Gelasius Mwalongo.

Maadhimisho hayo pia yameenda sambamba na sherehe za Yubilei ya miaka 25 ya Upadre, kwa mapadre wanne. Walioadhimisha Yubilei hiyo ni Padre Aidan Ulungi- Afisa Tawala Jimbo, Mkurugenzi wa Shirika la Kipapa la Utoto Mtakatifu Jimbo, pia ni mkurugenzi wa shule za Mt. Dominiko Savio zilizoko Jimboni Iringa, Padre John Mlomo Paroko wa Parokia ya Kilolo na Mkurugenzi wa Uchungaji Jimbo, Padre Romulo Mkongwa Paroko wa Parokia ya Mgololo na mlezi wa Radio Maria Jimbo Katoliki la Iringa, pamoja na Padre Joseph Magani kutoka Jimbo Katoliki la Lindi – mhadhiri wa Chuo kikuu cha Kikatoliki Ruaha ( RUCU)

Pichani kutoka Kulia: Pd. John Mlomo , Pd. Aidani Ulungi na Pd. Romlo Mkongwa.

Ibada ya maadhisho hayo yamehudhuriwa na mapadre zaidi ya 100 kutoka ndani na nje ya Jimbo la Iringa, watawa wa kike na kiume, pamoja na waamini walei kutoka ndani na nje ya Jimbo la Iringa.

Similar Posts

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *